Mambo Makuu Manne ya Kuzingatia ili Kufanya Upimaji Endelevu Wenye Tija-Sehemu ya Pili


Mambo makuu ya kuzingatia ili kufanikisha upimaji endelevu wenye tija. Picha: Mwandishi wa Makala.
Hakuna mjadala kuwa upimaji endelevu ni sehemu muhimu sana wakati wa mchakato wa kufundisha na kujifunza. Taarifa za namna ufundishaji na ujifunzaji unavyokwenda zinategemewa kupatikana kupitia upimaji endelevu bora.

Makala haya yanalenga kuendelea kujadili mambo makuu manne kama tulivyoyaona katika makala iliyotangulia. Mambo hayo ni ufafanuzi wa kina wa mambo makuu yanayopaswa kujifunzwa na wanafunzi (clarifying learning), kuwajengea wanafunzi ari ya kujifunza (activating learners), kutoa mrejesho wa maendeleo yao (providing feedback) na kutafuta ushahidi wa ujifunzaji (eliciting evidence of learning).

Katika makala haya nitajadili utoaji wa mrejesho wa Shughuli za Ujifunzaji (providing feedback) na utafutaji wa ushahidi wa ujifunzaji (Eliciting evidence of learning).

Kutoa Mrejesho wa Shughuli za Wanafunzi (Providing Feedback)
Kila anachokifanya mwanafunzi, anatamani sana kupata mrejesho wa usahihi wa anachokifanya. Hivyo, kutoa mrejesho wa yale wanayoyafanya wanafunzi darasani ni moja ya mambo yanayoweza kuwapa hamasa kubwa sana wanafunzi.

Utoaji wa mrejesho huwapa wanafunzi fursa ya kufahamu wanachopaswa kuendelea kukifanyia kazi. Hii huwasaidia wanafunzi kuzingatia kufanya mambo muhimu tu yanayolenga kufikia malengo yao ya ujifunzaji.

Utoaji wa mrejesho ni pamoja na mwalimu kufanya kazi na wanafunzi bega kwa bega ili awasaidie kufahamu vyema shughuli zao na kuwapatia taaarifa na ushauri sahihi wa namna wanavyoweza kukamilisha shughuli hizo.

Mwaka 2014 mtafiti Diane Gunlock alijaribu kuangalia umuhimu wa utoaji wa mrejesho kwa wanafunzi wa darasa la awali. Katika utafiti wake, Diane aligundua kuwa utoaji wa mrejesho husaidia hutoa hamasa ya wanafunzi kuhamasika kushiriki zaidi kwenye ujifunzaji, hali inayosaidia wanafunzi kupata kwa urahisi ujuzi unaokusudiwa.

Ushiriki wa dhati wa wanafunzi una manufaa makubwa sana. Wanafunzi wanaposhiriki kikamilifu kwenye ujifunzaji wao, mbali na kupata fursa ya kujifunza maudhui yaliyokusudiwa, hujifunza stadi nyingine za muhimu kwenye karne hii ya 21. Stadi hizo ni pamoja na namna bora ya kuwasiliana kupitia maongezi, maandishi, n,k, kutatua changamoto, kufikiri kwa kina na ubuninifu. Hiki ndicho kiini na hamasa kubwa sana ya mabadiliko ya mitaala kwa shule za Msingi, Sekondari na Vyuo vya ualimu yaliyofanyika kati ya mwaka 2005 na 2007.

Katika mapitio yao ya tafiti mbalimbali yaliyolenga kufahamu tafiti zinasemaje kuhusu namna bora ya utekelezaji wa upimaji unaomzingatia mwanafunzi, Rust, Price na O'Donovan (2005) walipata ushahidi usio na shaka kuwa utoaji wa mrejesho ndilo jambo la muhimu kabisa lenye tija kwenye ujifunzaji wa mwanafunzi.

Pamoja na kugundua hili, Rust, Price na O'Donovan walipata pia baadhi ya tafiti zilizoonesha kuwa utoaji wa mrejesho hakuwa na maana kwa baadhi ya wanafunzi. Wanaripoti kuwa, wakati baadhi ya wanafunzi waliohojiwa katika tafiti walisema hawaoni faida yoyote ya kutoa mrejesho ama ni kwa mara chache sana, utafiti mwingine ulionesha kuwa, pamoja na walimu kutoa mrejesho, wanafunzi hawaufuatilii kabisa.

Hata hivyo, watafiti hawa wanakiri matokeo hasi ya mrejesho wa ujifunzaji hutokana na namna zisizoridhisha za utoaji wa mrejesho huu. Ili kuhakikisha mrejesho wa shughuli wanazofanya wanafunzi unakuwa na manufaa, Rust, Price na O'Donovan wanapendekeza mambo makuu matatu ya kuzingatia. Mambo hayo ni;
  • Kuwasaidia wanafunzi kupata uelewa wa kutosha wa vigezo vya upimaji na viwango vya utendaji (knowledge of the performance standards)
  • Uwezo wa wanafunzi kulinganisha kazi zao na vigezo vya upimaji na viwango vya utendaji (comparing their work against the assessment criteria and performance standards)
  • Kuwasaidia wanafunzi kufanyia kazi tofauti walizogundua kati ya vigezo vya upimaji na viwango vya utendaji
Kwa uchambuzi wa kina wa namna walimu wanavyoweza kutumia mrejesho wenye tija, husuani kwenye ujifunzaji na upimaji unaomzingatia mwanafunzi, unaweza kuwsoma aidi hapa watafiti hawa Rust, Price na O'Donovan katika andiko lao lililolenga kupitia tafiti mbalimbali ili kubaini namna bora ya kutekeleza upimaji unaomzingatia mwanafunzi.

Kutafuta Ushahidi wa Ujifunzaji wa Wanafunzi (Eliciting evidence of learning)

Kutafuta ushahidi wa ujifunzaji wa wanafunzi n dicho kiini hasa cha upimaji endelevu. Lengo kuu ni kufahamu wanafunzi wamefikia wapi katika harakati zao za kufikia malengo mahususi ya ujifunzaji.

Katika upimaji endelevu, ukusanyaji wa taarifa zinazolenga kutoa ushahidi wa kutokea kwa ujifunzaji hufanyika kwa kila hatua ya somo. Ndio maana kipengele cha upimaji kimeongezwa kwenye maandalio ya masomo chini ya ufundishaji na ujifunzaji unaomzingatia mwanafunzi.

Zipo namna mbalimbali zinazoweza kutumiwa katika kukusanya ushahidi wa ujifunzaji wa mwanafunzi. Toleo la mwaka 2013 la maelezo ya mitaala ya shule za sekondari inayoakisi ufundishaji unaomzingatia mwanafunzi linaainisha njia kadhaa za namna bora ya kukusanya ushahidi wa ujifunzaji wa wanafunzi.

Njia mbalimbali zinazoweza kutumika kukusanya ushahidi wa ujifunzaji ni pamoja na matumizi ya majadiliano, midahalo, maswali na majibu, mikoba ya kazi, rubrics, rating scales, orodha hakiki, kazi mradi, majaribio kwenye maabara, insha na kadhalika.

Lengo la kutafuta ushahidi wa ujifunzaji unaofanyika kila hatua ya somo au mara kwa mara ni kufahamu wanafunzi wamefikia wapi na yapi yanawakwamisha ujifunzaji. Mchakato huu hutoa fursa kwa mwalimu (akishirikiana na wanafunzi) kutatua changamoto na kuweka mikakati ya kufikia malengo ya ujifunzaji yaliyokusudiwa.

Jambo la msingi la kukumbuka ni kuwa, ukusanyaji wa ushahidi wa ujifunzaji wa mwanafunzi hufanyika kwa kila hatua ya somo na ni endelevu. Uendelevu huu wa upimaji huwa na maana sana pale wanafunzi wanaposhiriki kikamilifu wakati wa ujifunzji wao.

Ndio maana, moja ya mambo ya msingi kabisa yanayosisitizwa ni kuchochea na kuamsha ari na hamasa ya wanafunzi kushiriki kwenye ujifunzaji. Hata hivyo, ushiriki wa dhati wa wanafunzi huchagizwa kwa ufanishi wa kiwango cha juu ikiwa wanafunzi watasaidiwa na mwalimu wao kufahamu kwa kina malengo makuu na mahususi ya ujifunzaji wao.Comments

Popular posts from this blog

Mambo Makuu Manne ya Kuzingatia ili Kufanya Upimaji Endelevu Wenye Tija

Mambo Muhimu ya Kuzingatia Katika Kuboresha na Kuongeza Ufanisi wa Shule.