Kujifunza Kujifunza ni Stadi Mama ya Stadi Zote
 Picha kutoka tovuti ya campaignforlearning

Tamko na 3.1.3 la Sera ya Elimu na Mafunzo, 2014 linaweka bayana kuwa elimu ya msingi ni ya lazima na inaishia kidato cha Nne. Tamko 3.1.5 linasisitiza pia kuwa, elimu hii katika mfumo wa umma itatolewa bure. Hizi ni nia njema kabisa na za kupongezwa. Si haba kuwa, hadi sasa utekelezaji wake unafanyika. Hata kama ni kwa taratibu au usio wa kiwango cha kuridhisha. 

Swali (pengine la msingi) la kujiuliza ni kuwa, elimu hii ya msingi inatoa msingi kweli kweli na je Sera inaeleza bayana msingi unaopaswa kutolewa?
Sera inaweka bayana matarajio ya ubora wa elimu na mafunzo kuanzia elimu ya awali hadi chuo kikuu. Kwamba, elimu na mafunzo yatakayotolewa yawe ni ya “viwango vya ubora unaotambulika kikanda na kimataifa na kukidhi mahitaji ya maendeleo ya Taifa” (uk 24). 

Mwanafunzi kutoka katika elimu yenye viwango na ubora unaozungumzwa hapo juu awe na sifa zipi? Sera ya Elimu na Mafunzo, 2014 imeweka bayana kabisa matarajio haya. Tamko namba 3.2.5 linasema, ninanukuu:
Serikali, kwa kushirikiana na wadau, itahakikisha mitaala inazingatia stadi za msingi za mawasiliano, kusoma, kuandika na kuhesabu; kutafiti; kuchambua taarifa; kutafsiri, kutathmini na kutumia maarifa, uvumbuzi, ubunifu na ujasiriamali katika ngazi zote za elimu na mafunzo.

Kwamba, kwa vyovyote vile, mwanafunzi anayepitia kwenye mfumo wa elimu wa Tanzania anatarajiwa kuwa na uwezo wa kuwasiliana vyema, kuwa mbunifu, mtafiti, mchambuzi makini wa taarifa, uvumbuzi n.k. Kwa hakika, soko la ajira linahitaji watu wa namna hii. Iwe kwa kujiajiri ama kuajiriwa.

Ukiacha stadi za kuhesabu, kusoma na kuandika, hizi stadi nyingine zinafundishwa wapi au ni wapi zinajitokeza wakati wa kujifunza? Kupitia Sera ya elimu na Mafunzo, Serikali imeweka lengo la kuwa na mazingira bora ya kufundishia na kujifunzia. Katika lengo hili, tamko namba 3.2.9, linasema, ninanukuu;

Serikali itahakikisha vifaa, nyenzo na zana stahiki za kufundishia na kujifunzia katika elimu na mafunzo zinatosheleza kulingana na mahitaji na maendeleo ya sayansi, teknolojia na mbinu za kufundishia na kujifunzia katika ngazi zote.

Hata hivyo, tusisahau msemo wa wahenga, kuwa, penye miti mingi hapana wajenzi. Mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji yanaweza kuwa bora kabisa lakini matarajio ya viwango wa vya ubora wa elimu unaotarajiwa yasionekane. Tunao wasimamizi wa elimu wanaoweza kutafsiri kwa ufasaha matakwa ya miongozo ya elimu ikiwamo sera hii? Kwa mfano, ni walimu wangapi wanachukua muda wao kusoma Sera ya Elimu wanayoitekeleza?

Ikiwa ubunifu, uchambuzi wa kina wa taarifa, utafiti, uvumbuzi si msomo ya moja kwa moja kwenye mitaala hususani kwenye elimu ya msingi, wanafunzi wanazipatia wapi stadi hizi muhimu katika karne hii na karne zinazokuja? Walimu wanazifahamu na kutambua umuhimu wa stadi hizi kwenye soko la ajira?

Kimsingi, bado tunakosa stadi ya msingi sana ambayo ni mama wa stadi zilizoainishwa kwenye sera ya elimu na mafunzo. Kujifunza kujifunza au kwa lugha rahisi kujifunza namna ya kujifunza. Ukosefu wa stadi hii ni donda sugu linalotumaliza watanzania kuanzia ngazi ya viongozi wakuu na kila mmoja wetu.

Kujifunza namna ya kujifunza kunamfanya mtu kuwa na tabia ya ujifunzaji endelevu (lifelong learning). Hakuna kitu ambacho maisha yote kitaendelea kuwa kama kilivyo. Kwamba, ukishakijifunza, ndio kitaendelea kuwa hivyo milele. Kukumbatia hali hii kunatufanya kuwa watu wa kufanya mambo kwa mazoea na hivyo kuzuia mabadiliko chanya hata mazingira yakiwa rafiki kwa kiasi gani.

Stadi ya kujifunza kujifunza kama nilivyodokeza awali, inamfanya mtu kuwa mjifunzaji mwendelevu. Bila kuwa na tabia ya ujifunzaji endelevu, si rahisi kuwa mbunifu, mtafiti, mchambuzi wa kina, na mvumbuzi. Tatizo hili linatuathiri vibaya sana kwenye utendaji wetu wa kila siku kwa namna mbalimbali.

Kuwa na kipaji haimaanishi kuwa itafika mahali bila juhudi yoyote utaweza kukitambua na kukifanyia kazi. Inahitajika juhudi ya kukitambua, kukifanyia kazi na kukiendeleza. Kuhitimu masomo, haimaanishi kuwa yale uliyojifunza shuleni, utayakuta kama yalivyo kazini.

Katika mazingira kama haya, kuna jambo la ziada linahitajika. Kwanza, kuwa na stadi ya kujifunza kujifunza. Stadi hii inatoa fursa ya kuwa tayari kujifunza kulingana na mazingira. Hii inakaribisha ubunifu, uvumbuzi, utafiti, kufikiri kwa kina alimradi kukabiliana na changamoto. Huku ndiko kujifunza kunakohitaji uwezo wa kujua namna ya kujifunza.

Tukihitaji ufanisi wa vijana wa umri chini ya miaka 17 kwenye mpira wa miguu kwa mfano, haitoshi tu kuwatumia kwa kuwa wana vipaji. Wanahitaji elimu inayoelezwa kwenye sera ya elimu na mafunzo, 2014. Wanahitaji ubunifu, tafakari pana, uvumbuzi, n.k. Mambo ambayo ikiwa hawana ujuzi/ stadi ya kuwa tayari kujifunza na kujifunza namna ya kujifunza, hatutokaa kuona mafanikio ya kusonga mbele yanayotarajiwa kutoka kwako. Itakuwa kawaida tu nap engine ule msemo wa kichwa cha mwendawazimu utaendelea kushamiri.

Elimu ya msingi ni kila kitu, hivyo iwe ya msingi kwelikweli. Ni muhimu kuelewa misingi mikuu inayopaswa kuwekwa ni ipi. Ubunifu, uwezo wa kuwasiliana, uvumbuzi, utafiti, uchambuzi, utumiaji wa maarifa n.k ni miongozi mwa mambo yanayotarajiwa kwenye elimu yetu msingi. 

Juu ya yote, stadi ya kujifunza namna ya kujifunza ni mama wa stadi zote. Ni moja ya misingi muhimu wanayopaswa kujengewa watoto na wanafunzi wetu. Ujifunzaji endelevu ni matokeo ya stadi na ujuzi wa kujifunza kujifunza. Msingi huu utawasaidia wanafunzi katika ngazi za elimu zinazofuta na hivyo kuwaandaa kuwa wanafunzi endelevu, kuwa na ufanisi kazini, kuweza kujiari na hatimaye kuleta tija kwenye jamii, kitaifa na kimataifa.

Comments

Popular posts from this blog

Mambo Makuu Manne ya Kuzingatia ili Kufanya Upimaji Endelevu Wenye Tija

Mambo Muhimu ya Kuzingatia Katika Kuboresha na Kuongeza Ufanisi wa Shule.

Mambo Makuu Manne ya Kuzingatia ili Kufanya Upimaji Endelevu Wenye Tija-Sehemu ya Pili