Njia Nne za Kutumia Ufundishaji na Ujifunzaji Unaomzingatia Mwanafunzihttps://1.bp.blogspot.com/-l6-3y-6h-3c/WJgcYNHBg_I/AAAAAAAAAfU/J1ACBYkuAxoTJ_CfJufoe826b4K5Dq9zACLcB/s320/Blogger_Picture%255B1%255D.jpg
Wanafunzi wa Chuo Cha Ualimu Mpwapwa wakishiriki kwenye moja ya shughuli za ujifunzaji darasani. Picha na Mwandishi wa Makala haya. 
Katika Makala zilizotangualia, nimekuwa nikijadili kuhusu elimu inayomzingatia mwanfunzi, hususani ujifunzaji wa kiudadisi. Makala ya kwanza ilijadili kuhusu maana, faida na namna ujifunzaji wa kiudadisi unavyoweza kutumiwa mashuleni.  Makala ya pili ililenga kujadili mbinu zinazoweza kutumiwa kujenga utamaduni wa ufundishaji na ujifunzaji wa kiudadisi mashuleni.  Makala ya tatu kwa upande mwingine, ilijadili namna mfumo wa sasa wa ufundishaji mashuleni unavyowanufaisha walimu kuliko wanafunzi. 

Makala haya yanalenga kujadili njia nne ambazo walimu na wawezeshaji wengine wanaweza kuzizingatia ili kuwezesha kwa kufuata misingi ya ujifunzaji wa kiudadisi. Njia hizi zitakazojadiliwa kwa kina ni Kuwamilikisha somo wanafunzi, mwalimu kuongea kwa kiasi na kuuliza maswali zaidi, kusisitiza uthibitisho wa hoja za wanafunzi na mwalimu kuwa na udadisi zaidi dhidi ya hoja za wanafunzi.
Njia ya Kwanza: Wafanye Wanafunzi Walimiliki Somo
Katika hatua hii, kuna nambo matatu ya msingi ambayo mwalimu anapaswa kuyafanya. Kwanza mwalimu anapaswa kujenga uhusiano imara na wa kuaminika kati yake na wanafunzi. Kuhakikisha kuna uhusiano mzuri sana miongoni mwa wanafunzi wenyewe. Kusiwe na ubaguzi wowote miongoni mwan wanafunzi-kiuwezo darasani, kiuchumi n.k. 

Wanafunzi waheshimiane na waone kila mmoja ana wajibu kwa menzake. Jambo la tatu ni kujenga utayari mzuri wa wanafunzi kitabia, kihisia na kiakili kwenye somo husika au shughuli za ujifunzaji.
Kujenga utayari wa wanafunzi kunaweza kufikiwa vizuri pale mwalimu anapotambulisha somo. Anaweza kuanza kwa simulizi fulani ya kusisimua inayoendana na somo. Pia, ni muhimu mwalimu akawaongoza wanafunzi kutambua umuhimu wa somo/ shughuli ya ujifunzaji katika maisha yao ya kila siku. 

Mazingira haya yanaweza kujenga utayari wa  mwanafunzi kitabia, kihisia na kiakili  wakati wa ujifunzaji wake. Kwa ujumla, ni wajibu wa mwalimu kutafuta namna ya kuchochea hamasa ya wanafunzi kushiriki katika somo wakiwa na utayari wa kiakili, kihisia na kitabia. 
Njia ya Pili: Mwalimu, Uliza zaidi, Ongea kwa Kiasi
Elimu inayomzingatia mwanafunzi, inamtaka mwanafunzi awe mtendaji mkuu. Mwalimu ni mzimamizi wa utendaji wa mwanafunzi. Hivyo, mwalimu anapaswa kufahamu ni wakati gani anapaswa kuongea na kwa kiasi gani. Kimsingi, mwalimu anapaswa kuwekeza kwenye kuuliza maswali yatakayowaibulia wanafunzi hamasa ya kujifunza zaidi. 
Ili mwalimu asitawale sana darasa hana budi pia kuhamasisha majadiliano na maongezi miongoni mwa wanafunzi. Wanaweza kufanya majadiliano katika vikundi au maongezi ya darasa zima. Pia, mwalimu awaongoze wanafunzi kuuliza maswali yanayotia hamasa ya kuendelea kujifunza. 
Njia ya Tatu: Hamasisha Wanafunzi Kuwajibika kwa Maoni Yao
Utaratibu huu ni mzuri kwani kwani utawafanya wanafunzi kujibidisha kujifunza kutoka vyanzo mbalimbali. Mbali na hili, utawajengea wanafunzi utaratibu wa kuwa makini na vyanzo vy aujifunzaji wanavyovitumia. Tena, utaratibu huu unaweza kuwafanya kuvihifadhi vyanzo hivyo kwani wanajua fika wana wajibu wa kutetea mitazamo yao. 
 
Mwalimu anaweza kuuliza mawali ya kumtaka mwanafunzi athibitishe kile anachokiamini na kukisimamia. Kwa mfano, anaweza kumuuliza mwanafunzi ni kwa nini anafikiri hivyo, amejuaje hicho anachokifikiri/ kisimamia na ikiwa ana uhakika na vyanzo/ chanzo cha maarifa anayoyaamini. 

Huu ni wakati ambao pia, mwalimu anapaswa kuwaongoza wanafunzi kurejea vyanzo mbalimbali, kufanya tafiti, kusoma vitabu n.k ili kuthibitisha au kukanusha yale wanayoamini ni sahihi au si sahihi. Pia, wakati huu, mwalimu anaweza kutoa uzoefu wake ambao unaweza kujadiliwa na wanafunzi kwa kuzingatia uzoefu wao na vyanzo vyao mbalimbali vya ujifunzaji
Njia ya Nne: Kuwa Mwenye Kutaka Kujua Zaidi Kutoka kwa Mwanafunzi
Njia hii inahusika zaidi na namna unavyoweza kupokea maoni wanayotoa wanafunzi ili kuwafanya wazidi kupata hamasa ya kujifunza. Penda kujua zaidi kwa kuwauliza wanafunzi maswali kuhusu hayo wanayoyaamini. Unaweza kumuuliza mwanafunzi ikiwa anaweza kufafanua zaidi, au darasa kujadili zaidi. Mwanafunzi apewe nafasi ya kutetea hoja yake. Pia, mwalimu asisahau kuthamini maoni ya wanafunzi. Hii itazidisha hamasa ya ujifunzaji wao. 
Hata hivyo, ni vizuri mwalimu akapangilia somo kulingana na mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji yaliyopo kwa kuzingatia dondoo hizi muhimu. Hatua hizi zinawezekana kenye mazingira yoyote. Ni namna ya uwezeshaji inayolenga kumfanya mwanafunzi kuwa kiini cha ujifunzaji wake. Hili ndilo jambo kubwa la kuzingatia. 
Mwalimu apangilie na ajiandae kuhusu namna atakavyowashawishi wanafunzi kushiriki kwenye somo wakiwa na utayari wa kitabia, kihisia na kiakili. Ni vyema mwalimu afahamu ni wakati gani atawaongoza wanafunzi kuuliza maswali makini yatakayowaongoza kutafiti, kudadisi na kuyapatia majibu maswali hayo. 

Mmwalimu anawajibu pia wa kujua ni wakati gani na kwa namna gani wanafunzi watawasilisha maoni yao yanayolindwa na ushahidi kutoka vyanzo vinavyoaminika. Misimamo ya hoja zao na namna wanavyotumia maarifa kulinda hoja zao kinaweza kuwa ni kiashiria cha kiwango cha ujifunzaji. 

Wakati huu, wanafunzi wanapaswa waweze kuwa na uwezo wa kujibu maswali yaliyowaongoza kwenye tafiti zao, uvumbuzi na udadisi na pia waweze kutumia maarifa haya kukabiliana na changamoto mbalimbali katika maisha yao ikiwezo kuwa na uwezo wa kutetea yale wanayoyaamini.

Comments

Popular posts from this blog

Mambo Makuu Manne ya Kuzingatia ili Kufanya Upimaji Endelevu Wenye Tija

Mambo Muhimu ya Kuzingatia Katika Kuboresha na Kuongeza Ufanisi wa Shule.

Mambo Makuu Manne ya Kuzingatia ili Kufanya Upimaji Endelevu Wenye Tija-Sehemu ya Pili