Mbinu za Kusaidia Kujenga Utamaduni wa Ufundishaji wa Kiudadisi Mashuleni                   Picha kutoka tovuti ya Linkedin
Moja ya changamoto zinazokwamisha matumizi ya ufundishaji wa kiudadisi mashuleni ni hali ya utayari wa walimu, wakuu wa shule, viongozi wa kisiasa na wadau wengine wa elimu. 

Changamoto kadhaa zinatajwa kukwamisha utekelezaji wa ufundishaji na ujifunzaji huu. Baadhi zikiwemo uhaba wa nyenzo za kujifunzia na walimu kukosa maarifa ya namna ya kutumia njia za ufundishaji zainazoendana na matakwa ya mfumo huu. 

Hata hivyo, katikaki ya changamoto hizi, bado utekelezaji wa ufundishaji na ujifunzaji huu unawezekana. Utayari wa wadau wa elimu ndio chachu pekee ya kufanikisha hili. Palipo na utayari, changamoto kama hizi huweza kuonwa kama fursa na kuzifanyia kazi na hatimaye kufanikisha utekelezaji wa ufundishaji unaowazingatia wanafunzi.

Ni heri mwalimu wa darasa la wanafunzi 50 aliye na kitabu kimoja na nia thabiti ya kutafuta namna ya kuwapa wanafunzi kitabu hicho wajifunzie, kuliko mwalimu wa darasa kama hilo aliye na vitabu kumi anayelalamikia upungufu wa vitabu kiasi kwamba asione hata umuhimu wa kuwapatia wanafunzi vitabu hivyo ambavyo yeye anaviona ni vichache.

maneno hapa juu yana maana moja kubwa. Utayari wa kufanya jambo ni nguvu inayoweza kukutengenezea njia ya kufanya mambo ambayo wengi huweza kuyaona yasiyowezekana. Nia ya dhati ya utekelezaji wake huweza kujengwa na wadau wenyewe wa elimu. Walimu, viongozi wa shule, wanafunzi, wazazi n.k. Katika Makala haya, mandishi analenga kujadili namna anuai za kusaidia kukuza utamaduni wa matumizi ya ufundishaji wa kiudadisi mashuleni.

Kujifunza na kuukubali mfumo huu kama muongozo wa utoaji elimu

Maisha ya jamii fulani huongozwa na misingi ambayo kila mwanajamii anaifahamu na anajua umuhimu wa kuifuata. Mfano mzuri ni imani. Ili uitwe mfuasi wa Imani fulani, ni sharti uwe unaifahamu na kuitekeleza misingi ya imani hiyo. 

Hali kadhalika, ikiwa shule inahitaji kuutumia mfumo huu, haina budi kuukubali kama msingi wa kusimamia na kuongoza utoaji wa elimu shuleni hapo. Kuukubali ni pamoja na kuuelewa vyema na kuweka mikakati thabiti ya namna ya kutekeleza.

Ni wajibu wa wasimamizi wa shule kuweka mikakati mahususi ya kupata maarifa ya utekelezaji wa ufundishaji wa kiudadisi unaoweza kufanyika kupitia mafunzo kabilishi kwa kuwasiliana na wataalam. Pia, mwalimu mmoja mmoja anaweza kupanua uelewa wake kupitia tovuti mbalimbali mitandaoni zilizo na maarifa yanayohusiana na ufundishaji wa kiudadisi. 
Ikumbukwe, yote haya yanawezekana palipo na utayari wa dhati usiobabaishwa na kukatishwa tamaa na changamoto za hapa na pale.

Wasimamizi wa shule kuwa na maono juu ya Ufundishaji wa Kiudadisi

Wasimamizi wa shule ni watu muhimu sana wa kufanikisha utekelezaji wa ufundishaji unaowazingatia wanafunzi. Wana mchango mkubwa kuhusu upatikanaji wa nyenzo za kujifunzia, rasilimali watu, fedha na motisha nyingine kwa walimu. 

Wasimamizi wa shule wana mchango mkubwa wa kiushawishi kwa watu wa chini yao. Hivyo, wanapaswa kuwa na maono ya mbali sana kuhusu namna wanavyoweza kufanikisha matumizi ya mchakato wa ujifunzaji wa kiudadisi. Wanapaswa kuwa na mipango thabiti na endelevu. Maono yatasaidia watekelezaji wa chini kuyasimamia kwa kuweka mipango thabiti ya utekelezaji.

Uwepo wa Wahamasishaji wakuu

Ni jambo la kawaida kabisa, wakati fulani pamoja na kuamua jambo kwa pamoja, kuna wakati hufika watu wakakata tamaa na kuona mambo hayawezekani. Ili kufanikisha hazma ya kutumia mfumo wa ufundishaji wa kiudadisi, inashauriwa kuwepo na watu walio na utayari thabiti.

Watu hawa watasaidia kutoa hamasa, kuonesha njia ili kuhakikisha hakuna kikwazo katika utekelezaji. Hata pale vikwazo vinapotokea, viweze kubadilishwa na kuwa fursa na hivyo kuendeleza utamaduni wa ufundishaji wa kiudadisi. 

Kutokukatishwa tamaa na Changamoto wakati wa utekelezaji

Hili ni jambo la muhimu sana. Miongoni mwa changamoto zinazosemwa  kukwamisha utekelezaji wa ufundishaji unaowazingatia wanafunzi ni kukosekana kwa hamasa miongoni mwa walimu. Hamasa zinazokosekana ni pamoja na mshahara mdogo, mazingira magumu ya kazi, pamoja na upungufu wa nyenzo za kujifunzia. Katika hali hii, kuna swali la kiufahamu linapswa kupatiwa majibu. 

Ikiwa walimu wanakosa hamasa, kwa nini wasiache kabisa kufundisha mashuleni na wakafanye mambo mengine yatakayowapa hamasa?
Hili si swali la dhihaka. Ninachopenda kukisisitiza hapa ni kuwa, kwa kuwa walimu wanaendelea kufundisha mashuleni, ni fursa yao adhimu kufikiri na kubuni namna ya kutumia mfumo huu wa ufundishaji. 

Kimsingi, hakuna wanachopoteza. pengine wanaopotea ni wanafunzi wanaofundishwa ka njia za kukariri maarifa na ambayo hayatawafaa sana maishani. Kukabiliana na changamoto ndio namna pekee ya kusonga mbele na kuhakikisha mfumo huu unafanikiwa. 

Nirudie tena kusisitiza kuwa, ni heri sana kwa mwalimu yule aliye na kitabu kimoja lakini ana nia ya dhati kabisa na anahaha kutafuta namna ya kufanya kitabu kile kimfikie kila mwanafunzi kuliko mwalimu aliye na vitabu kumi na hata asiweze kuwapatia wanafunzi wakavitumia. walimu wakisubiri wapate vitabu vitakavyomtosha kila mwanafunzi. Kwa hakika, tutasubiri milele.

Uaminifu miongoni mwa watekelezaji

Uaminifu wakati wa utekelezaji wa mchakato wa ufundishaji wa kiudadisi ni muhimu. Inapotokea baadhi ya watekelezaji kuwa na mawazo kinzani, ni dhahiri watu hawa watafanya kila hila kukwamisha utekelezaji. Uaminifu baina ya watekelezaji husaidia kuweka mipango ya pamoja, kutumia rasilimali vizuri na kuwa na mwisho unaofanana. 

Ushirikiano

Moja ya nyenzo muhimu ya kufanikisha ujifunzaji wa kiudadisi ni ushirikiano. Ushirikiano unaweza kuwa wa aina na ngazi tofauti. Ushirikiano baina ya wasimamizi wa shule/ elimu na watekelezaji wengine, ushirikiano baina ya walimu wa masomo na ushirikiano baina ya walimu na wanafunzi.

Katika ngazi ya ufundishaji madarasani, inapendeza sana walimu wa somo husika wakashirikiana. Ushirikiano unaweza kuanza wakati wa maandalizi. Maandalizi haya ni pamoja na kujenga uelewa wa pamoja sambamba na kupanga namna ya kufanikisha somo. Pamoja na maandalizi haya, walimu wanapaswa kutafakari njia bora watakazozitumia kuwapatia wanafunzi nyenzo za ujifunzaji. 

Ikumbukwe kuwa, wajibu wa mwalimu ni kusimamia ujifunzaji wa mwanafunzi. Usimamizi huu ni pamoja na kuhakikisha mwanafunzi anajifunza yale yaliyokusudiwa kwake kwa kupatiwa nyenzo sahihi zitakazofanikisha azma ya ujifunzaji wake.

Kuhakikisha Nyenzo za ujifunzaji zinapatikana

Jukumu la kuhakikisha rasilimali muhimu zinapatika mashuleni ni la kila mmoja kwa nafasi yake. Wasimamizi wa shule wana mchango mkubwa katika hili. Maadam msimamizi amekuwa na utayari na nia ya dhati, atahakikisha  nyenzo stahiki zinapatikana, hata kama ni kwa awamu. 

Wajibu huu pia, wanao walimu, wazazi, wanafunzi na wadau wote wa elimu. Kinachoongoza mafanikio ni utayari na nia. Mambo mengine kama nyenzo za ujifunzaji zitapatikana palipo na nia. Wakati mwingine hata hizo zinazoonekana hazitoshi zinaweza kutosheleza. 

Mahitaji ya nyenzo za kujifunzia, hata hivyo yanategemea na mpangilio wa somo wa mwalimu husika. Si kila mwalimu anahitaji mahitaji yanayofanana. 

Upatikanaji wa nyenzo za ufundishaji imekuwa ni moja ya changamoto kuu inayotajwa kukwamisha kufanikisha ujifunzaji wa kiudadisi. Hata hivyo, ikiwa walimu hawataanza kutumia nyenzo chache zilizopo, ni vigumu sana wadau wengine wa elimu kuona umuhimu wa kusaidia kupatikana kwa nyenzo zinazohitajika. 

Kila shule inaweza kuwa na mahitaji yake. Hivyo, ni muhimu pia, kila shule iweke mikakati ya kutekeleza ufundishaji huu kwa kutumia rasilimali chache zilizopo. 

Wazoefu wa utumiaji wa ufundishaji wa kiudadisi wanashauri walimu wajaribu kutumia rasilimali zinazoendana na mazingira yao. TEHAMA inaonekana ni kiungo muhimu katika kufanikisha ufundishaji wa kiudadisi. Hata hivyo, shule nyingi za Tanzania bado hazijakuwa na miundombinu rafiki. Pamoja na hali hii, walimu wanashauriwa kutumia rasilimali zilizopo bila kujali uchache wake.

Watekelezaji kuwa huru kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili

Hili ni jambo la muhimu, tena ndio kiini cha ufundishaji na ujifunzaji wa kiudadisi. Walimu wapewe fursa ya kutatua changamoto zinazowakabili pale inapowezekana. Mawazo yao yatambuliwe na yafanyiwe kazi. Hali kadhalika kwa wanafunzi, kwa kuwa wao ndio kiini cha ujifunzaji wao, wanapaswa kuwa pia sehemu ya kutatua changamoto zao za ujifunzaji. 

Utaratibu huu unawakuzia wanafunzi stadi za kiuvumbuzi na  kuweza kutatua changamoto mbalimbali. Hii ni sehemu muhimu inayowajengea uwezo wa kujisimamia kwenye ujifunzaji wao. Katika kujifunza, matatizo yao ni kiu ya kutaka kujifunza. Ili kukidhi kiu hii, ni lazima watafute mbinu, wafanye utafiti, wahoji, wahojiane, ili wajenge uelewa unaotakiwa.

Mwisho, ni rai yangu kwa wadau wote wa elimu, tuone umuhimu wa kutumia njia hizi za kuwaleta wanafunzi kwenye ujifunzaji wao. Walimu kuendelea kuwa chanzo kikuu cha maarifa kwa wanafunzi ni mfumo usio na tija yoyote zaidi ya kuwadumaza vijana wetu. Ikiwa tunahitaji taifa la wasomi wenye tija kwenye jamii, hatuna budi kuwekeza katika njia hizi za ufundishaji na ujifunzaji. 

Tusitegemee kijana asiyeweza kutambua wajibu wake katika ujifunzaji wake akapata elimu bora na itakayomfaaa katika maisha. Ataweza kujibu mtihani na atarudi nyumbani na elimu yake isimfae kabisa. Kuna uwezekano mkubwa akawa changamoto badala ya kuwa msaada katika jamii.

Uwezo na utayari wa kujiajiri na kuajirika unapaswa kujengwa kupitia namna mwanafunzi anavyojifunza. Ufundishaji wa kiudadisi unamsaidia kijana kukuza stadi za kudadisi, kuhoji, kuchambua na kufikiri kwa kina, miongoni mwa stadi muhimu kwenye karne ya 21 za kusaidia kuleta mageuzi chanya ya kiuchumi, kielemu na kijamii.


Comments

Popular posts from this blog

Mambo Makuu Manne ya Kuzingatia ili Kufanya Upimaji Endelevu Wenye Tija

Mambo Muhimu ya Kuzingatia Katika Kuboresha na Kuongeza Ufanisi wa Shule.

Mambo Makuu Manne ya Kuzingatia ili Kufanya Upimaji Endelevu Wenye Tija-Sehemu ya Pili