TPACK: Moja ya Maarifa Muhimu kwa Walimu 
Picha imetumiwa kwa ruhusa kutoka http://tpack.org     
TPACK ikiwa ni kifupisho cha Technological Pedagogical Content Knowledge, ni nadharia inayolenga kutoa ufafanuzi wa ujuzi anaopaswa kuufahamu mwalimu ili aweze kutumia TEHAMA kwa ufasaha katika ufundishaji wake.
Modeli hii inamkumbusha mwalimu kuhusu aina ya ujuzi anaotakiwa kuwa nao, ukiwamo wa kutumia Tehama katika ufundishaji. Kwa mujibu wa modeli hii, ujuzi huu upo katika sehemu kuu tatu ambazo ni Ujuzi wa ufundishaji (pedagogy), Ujuzi wa Maudhui ya somo (content knowledge) na Ujuzi wa tekinologia (Technological Knowledge) unaokusudiwa kutumiwa kwenye ufundishaji. 
 Hata hivyo, nadharia ya TPACK inaenda mbali zaidi kwa kuonesha pia namna ujuzi huu niliotangulia kuutaja unavyoingiliana na kutegemeana. Hii ni kusema, mwalimu akiwa na ujuzi wa kufundisha halafu hayajui vyema maudhui ya somo, ni sawa na kazi bure. Itamwia vigumu kufanikisha ufundishaji. 
Hali kadhalika,  kama mwalimu anauelewa mpana wa maudhui ya somo na hana ujuzi wa namna ya ufundishaji, ni dhahiri kuwa, kile anachokifahamu hataweza kukiwasilisha kwa wanafunzi kwa ufasaha. Kwa hiyo, modeli hii pia inawakumbusha walimu kuwa ujuzi wa ufundishaji na ujuzi wa maudhui (Pedagogical Content Knowledge-PCK) unapaswa kwenda sambamba.
Pia, mwalimu anapaswa kuwa na ujuzi wa namna ya kutumia tekinolojia katika ufundishaji. Kwa hiyo, ujuzi huu pia, lazima uende sambamba na ujuzi wa ufundishaji na ujuzi wa maudhui ya somo. Kwa maana hii, kuna ujuzi mwingine wa aina mbili unaoibuka ambao ni ujuzi wa ufundishaji unaokwenda sambamba na ujuzi wa kitekinolojia (Technological Pedagogical knowledge-TPK) na  ujuzi wa maudhui ya somo unaokwenda sambamba na ujuzi wa kitekinolojia (Technological Content Knowledge-TCK).   
Aina ya mwisho ya ujuzi unaopatikana katika modeli hii ni ule unaojumuisha ujuzi wa matumizi ya tekinolojia unaoenda sambamba na ujuzi wa ufundishaji pamoja na ujuzi wa maudhui ya somo husika, yaani Technological Pedagogical and Content Knowledge-TPACK. Maelezo hapa chini yanafafanua kila aina ya ujuzi anaopaswa kuwa nao mwalimu kama modeli ya TPACK katika picha hapo juu inavyoonesha.
Ujuzi wa Ufundishaji-Pedagogical Knowledge-PK
Maarifa ya ustadi wa ufundishaji yanajumuisha ujuzi mbali mbali alionao mwalimu wakati wa kufundisha. Mwalimu hujifunza mambo haya vyuoni  na pia kupitia uzoefu kazini. Ninaweza kuuita ujuzi huu kuwa ni Sanaa ya ufundishaji kwani, ndio ustadi wa kuwasilisha maudhui kwa wanafunzi. 
Ujuzi wa ufundishaji ni mjumuisho wa mambo mengi yakiwemo namna ya uandaaji wa somo, namna ya kuwashirikisha wanafunzi wakati wa somo, namna ya kuhakikisha darasa lina utulivu, namna ya kutahini na kutathmini wanafunzi, namna ya kutumia zana mbali mbali za ufundishaji n.k. Hii ni kusema kuwa, mwalimu anayekosa stadi hizi, itamwia vigumu sana kuwatimizia kile wanafunzi wanachopaswa kujifunza. Pia, mwalimu hataweza  kutumia tekinolojia ipasavyo katika ufundishaji wake.
Ujuzi wa Maudhui ya Somo Husika-Content Knowlegde-CK
Ujuzi wa Maudhui ya Somo ni mjumuiko wa maarifa aliyonayo mwalimu kwenye somo au mada anayoifundisha. Uelewa mpana wa maudhui ya somo pamoja na ujuzi wa ufundishaji humfanya mwalimu kufanikisha kwa ufasaha jukumu lake la ufundishaji.
Ujuzi wa tekinolojia-Technological knowledge-TC
Ujuzi wa kitekinolojia ni moja ya maarifa anayopaswa kuwa nayo mwalimu kabla ya kuamua kutumia TEHAMA kwenye ufundishaji. Ujuzi wa Tehama unajumuisha mambo mengi kama vile namna ya kutumia vifaa kama compyuta(na vitumizi vyake kama vile Microsoft office), projekta, modem, mtandao wa intaneti, n.k. Pia, ujuzi huu ni pamoja na uwezo wa kutambua umuhimu wa kutumia TEHAMA na namna inavyoweza kuboresha ufundishaji.
Ujuzi wa maudhui na Ufundishaji-Pedagogical content knowledge-PCK
Kufahamu vyema namna ya kufundisha  hakutoshi. Vile vile, kuwa na ufahamu wa kutosha wa mada mwalimu anayokusudia kuifundisha hakutoshi pia. Mwalimu anapaswa kuwa na ujuzi wa namna ya kufundisha pamoja na ujuzi mpana wa mada anayokusudia kuifundisha. Ufahamu mzuri wa Sanaa ya ufundishaji humuwezesha mwalimu kufundisha kwa ufasaha kile alichokusudia. Mwanafunzi wa kidato cha sita wa “part time” aliyepewa jukumu la kufundisha wanafunzi wa sekondari anaweza kuwa na ufahamu wa kutosha wa maudhui ya somo husika lakini akashindwa kuwaelewesha wanafunzi kwa sababu ya kukosa maarifa ya namna ya kufundisha.
Ujuzi wa Maudhui  na  wa Tekinolojia- Technological content knowledge-TCK
Ujuzi wa maudhui na tekinolojia ni muunganiko wa ujuzi wa kitekinolojia alionao mwalimu pamoja na ujuzi wa somo analofundisha. Mwalimu hana budi kufahamu umuhimu wa tekinologia katika ufundishaji na namna unavyoweza kumsaidia katika kuandaa, kuwashirikisha wanafunzi pamoja na kurahisisha uelewaji wa haraka na wa ufasaha kwa mwalimu mwenyewe na kwa wanafunzi.
Ujuzi wa ufundishaji na wa Kitekinolojia-Technological Pedagogical Knowledge-TPK
Mwalimu bora wa ulimwengu wa sayansi na tekinolojia ni yule aliye na maarifa ya kutosha ya sanna ya ufundishaji pamoja na ujuzi wa kitekinolojia, husani inayohusiana na ufundishaji. Mwalimu hana budi kuwa na ufahamu wa namna anavyoweza kutumia tekinologia pamoja na mbinu za ufundishaji ili kurahisisha uelewaji wa somo kwa wanafunzi.
Mwalimu anapaswa kufahamu ni wakati gani anapaswa kutumia zana ya kidigitali, kwa nini na ni kwa namna gani wanafunzi watashiriki kuitumia ili kurahisisha ufundishaji. Kwa mfano, mwalimu anayetumia kompyuta na projekta kuwapitisha wanafunzi tu kwenye nukuu alizoandaa inaweza kuhesabiwa kuwa siyo namna muafaka sana hususani kwa wanafunzi wa elimu ya chini kama sekondari. Hapa vifaa hivi vya kitekinolojia vitakuwa vinamrahisishia (kwa kiasi fulani) mwalimu peke yake, na siyo wanafunzi.
Kimsingi, vifaa na zana za kitekinolojia zinapaswa kumsaidia mwanafunzi kuelewa kwa urahisi dhana ambazo katika hali ya kawaida ni vigumu kuzielewa. Zana hizi ni kama vile mada za mifumo mbali mbali ya binadamu na wanyama kama vile ya upumuaji, utoaji taka, michakato ya kikemikali, masuala ya anga za juu n.k. 
Siyo rahisi watoto kufika anga za juu, au kuona namna mfumo wa upumuaji unavyofanya kazi kwa wanyama au binadamu. Kupitia zana za kidigitali kama vile video na aninmations, wanafunzi wanaweza kujifunza kwa kuukaribia uhalisia wa nadharia wanazojifunza, na hivyo kuzielewa kwa haraka na kwa ufasaha.
Ujuzi wa Tekinolojia katika Ufundishaji wa Maudhui- Technological pedagogical content knowledge-TPCK
Kuwa na ujuzi wa kufundisha bila ujuzi wa maudhui ya somo husika hufifisha kiwango cha uelewaji wa wanafunzi. Wapo walimu wengi wasio na uelewa mpana wa kile wanachofundisha. Hali hii hupelekea wanafunzi kushindwa kujifunza kwa ufasaha kile walichopaswa kujifunza. Mara nyingine wanafunzi hulazimika kuelewa dhana potofu kwa sababu ya uelewa mdogo wa mwalimu kwenye mada husika.
Kuwa na maarifa ya ufundishaji sambamba na yale ya maudhui kunaweza pia kusilete ufanisi katika ufundishaji. Kuna mada ambazo hata mwalimu awe na ujuzi wa kutosha wa ufundishaji na wa maudhui, bado anaweza asieleweke vyema na wanafunzi katika mada fulani. Zipo mada ambazo ni za kufikirika zaidi. Kutumia ubao, maabara na zana zitokanazo na mazingira yetu zinaweza zisirahisishe uelewaji wa mwanafunzi. Hivyo, mwalimu na wanafunzi kulazimika kupata msaada zaidi na hapa ndipo walimu na wanafunzi wanapopaswa kutambua umuhimu wa tekinolojia katika ufundishaji.
Tekinolojia huweza kumrahisishia mwalimu katika kufundisha mada ngumu. Mada ambazo katika mazingira ya kawaida asingeweza kuwafundisha wanafunzi wakaelewa. Kwa mfano, mada kama za Baolojia kama vile mifumo ya homoni, damu na namna ogani mbalimbali zinavyofanya kazi huweza kujifunzwa kwa urahisi zaidi kwa kutumia video na animations zinazoonesha uhalisia wa kinachotokea. Michakato ya kikemikali katika somo la kemia huweza kufafanuliwa kwa ufasaha zaidi kwa kutumia tekinolojia kuliko mwalimu anavyoweza kufafanua.
Hivyo basi, kutokana na umuhimu wa tekinolojia katika ufundishaji, mbali na walimu kuwa na ujuzi wa ufundihaji na ule wa maudhui, hawanabudi pia kuwa na uelewa wa kutosha wa tekinolojia. Hii ina maana kuwa, mwalimu katika zama hizi za sayansi na tekinolojia anapaswa kuwa na ujuzi wa kitekinolojia katika ufundishaji wa maudhui yanayokusudiwa.
Bado kuna changamoto kubwa kwa upande wa walimu, ya kutokuwa na utayari wa kutumia maarifa haya ya tekinolojia za kisasa kwenye ufundishaji na ujifunzaji. Walimu wana nafasi kubwa pia ya kumjengea mwnafunzi tabia ya kutumia vizuri tekinolojia hizi za kisasa, hususani katika ufundishaji na ujifunzaji .
Tatizo jingine lipo vyuoni, kule wanapopikwa walimu. Mafunzo ya TEHAMA hufundishwa kwa nadharia. Hata nadharia yenyewe inafundishwa kwa ujumla, siyo ile ya kumsaidia mwalimu kuweza kuitumia moja kwa moja TEHAMA katika ufundishaji na ujifunzaji. Hakuna budi utaratibu huu kubadilishwa. Kama tatizo ni upungufu wa vifaa kama vile kompyuta, kwa elimu ya vyuo vikuu, mathalani,  kupitia fedha ya mkopo wa elimu ya juu,  kila mwanafunzi anaweza kuwa na uwezo wa kumiliki kompyuta yake. Suala hili lingewekwa kuwa ni la lazima, kila mwanafunzi anapoanza mwaka wa kwanza ni lazima awe na Kompyuta. Kwa namna hii, ufundishaji wa TEHAMA ungekuwa ni wa vitendo zaidi, kuliko nadharia ya sasa.
Ni rai yangu kwa walimu, ulimwengu sasa umekuwa kama kijiji. Darasa siyo lazima liwe lile lenye ubao, chaki na kuta nne. Sayansi na tekinolojia imerahisisha upataji wa habari. Popote pale walimu tunaweza kujifunza. Jikoni, sebuleni, chumbani na hata baa kunaweza kuwa darasa.
Tusisubiri semina za mafunzo kazini za mitaala mipya. Hata walioandaa mitaala mipya waligugo, wakajiongezea maarifa, wakaandaa mtaala. Nasi walimu hatuna budi kujiongeza. Semina zote tunazolia hatujazipata, tunaweza kujifunza wenyewe. Hima tuamke, tuwe mfano mzuri kwa wanafunzi. Vijana wa sasa tunasema, hatuna budi “kujiongeza”. 
Tusisubiri kupewa kwanza "posho" ndio tujifunze, tuamini kuwa, mafunzo yenyewe ndiyo "posho" ya msingi. Kwa namna hii, kamwe hatutasubiri mafunzo kabilishi, tutaendelea kujituma kujifunza kile tunachoona tunahitaji kukifahamu ili kufanikisha lengo la ufundishaji. Tutumie TEHAMA, ina kila tunachofikiri tunahitaji kukifahamu katika ufundishaji na ujifunzaji.


Comments

Popular posts from this blog

Mambo Makuu Manne ya Kuzingatia ili Kufanya Upimaji Endelevu Wenye Tija

Mambo Muhimu ya Kuzingatia Katika Kuboresha na Kuongeza Ufanisi wa Shule.

Mambo Makuu Manne ya Kuzingatia ili Kufanya Upimaji Endelevu Wenye Tija-Sehemu ya Pili