Ni Kukua kwa Kiswahili, Kuporomoka au ni Mwanzo wa lugha Nyingine?

Pamoja na kuwa Kiingereza ndio lugha rasmi ya kufundishia katika shule za sekondari na vyuo vikuu, ni muda mrefu sasa kumekuwa na mijadala ya lugha ipi kati ya hizi mbili ni muafaka katika kufundishia. Mijadala hii inakuja kufuatia kuendelea kudorora kwa ubora wa elimu nchini Tanzania. Kuhusiana na hili, tafiti nyingi zimeshafanyika. Lengo si kujadili tafiti hizi, wala ni lugha ipi ni muafaka katika kufundishia wanafunzi nchini Tanzania. Hii inaonesha kuwa Tanzania tuna utata katika matumizi ya Kiswahili na Kiingereza. Utata unaohitaji suluhisho.
Watanzania tulio wengi tumekuwa na tabia ya kuchanganya lugha ya Kiswahili na kiingereza katika kuongea. Bahati mbaya sana wengi wa watumiaji wa mseto huu ni wasomi  au waswahili waliopata bahati ya kujua maneno machache ya kiingerezaa au ni waongeaji wazuri wa Kiingereza.
Kwa mtazamo wangu, hili ni tatizo letu watanzania. Tena ni tatizo la msingi kabisa. Kiswahili ni moja ya utambulisho wetu watanzania. Huu ni utambaduni wetu. Tunapochanganya Kiswahili na kiingereza, tunaupoteza utamaduni wetu. Tunaidharau fahari yetu.
Sentensi moja inapoundwa kwa Kiswahili na kiingereza, sidhani kama mhusika atatambulika kuwa anaongea Kiswahili au Kiingereza. Bila shaka hii ni lahaja mpya kabisa. Mfano wa mseto ni kama vile Leo ninataka kukutoa out, infact utaratibu huu si mzuri, you messed up ndugu yangu, huyu ndiye girlfriend wangu, unajua issues kama hizi hazisound kabisa n.k . Haya ni mazoea mabaya katika matumizi ya Kiswahili.
Watanzania tunaelekea kupata lugha mpya ambayo bado tutajinadi nayo kuwa  ni Kiswahili. Sidhani kama tutajivunia kuwa tumejenga Kiswahili. Mwisho wa siku, tutajikuta tunaongea Kiswahili kilicho na viraka vya maneno ya Kiingereza au kilichobandikwa maneno mengi ya Kiingereza (na lugha nyingine).
 Cha kushangaza ni kuwa, maneno mengi ya kiingereza yanayotumiwa katika sentensi za Kiswahili yana maneno ya Kiswahili yaliyo rahisi kabisa na yaliyozoeleka. Wazungumzaji, wataalam  na wadau wengine wa lugha ya Kiswahili wanapaswa kuliona hili na kulisemea.
Ninatambua kuwa, moja ya namna ya kukua kwa lugha, ni kukopa maneno kutoka katika lugha nyingine. Ni dhahiri kuwa, Kiswahili ni moja ya lugha zilizokwisha kopa maneno mengi kutoka katika lugha nyingine. Lakini, namna watanzania tunavyochanganya lugha wakati wa kutumia kiingereza siyo namna sahihi ya kukikuza Kiswahili.
Ni kweli kuwa watanzania huwa tunakosa maneno ya Kiswahili hadi tuamue kutumia kiingereza au ndio ustaarabu tulioamua kuuishi? Sidhani kama hali ndio hii, na ukweli utabaki kuwa huu ni utaratibu tunaojijengea pamoja na kuwa tuna uwezo wa kuongea Kiswahili bila kuchanganya na Kiingereza.
 Kama ni kweli huwa inafika mahali tunakosa neno sahihi la Kiswahili,  tunajibidisha kujifunza kwa kutafuta maneno hayo sahihi ili wakati mwingine tusirudie makosa haya? Kushindwa kufanya hivi ni moja ya dalili za kutokujitambua na tusio elewa wajibu wetu wa kukitunza na kukikuza Kiswahili kama watumiaji wakuu barani Afrika na Duniani kote.
Swali la kujiuliza ni kuwa,  katika kuzungumza, ni kweli tumejihakikishia kuwa hakuna maneno ya Kiswahili ambayo yangeweza kusimama badala ya neno au maneno ya Kiingereza yaliyotumiwa? Huku ni kwenda na wakati, ni kuvuta hadhira, ni mkakati wa kukikuza Kiswahili au ni nini? Tutafakari kwa pamoja kilema hiki kilicho miongoni mwa watanzania wa sasa na wanaoaminiwa kuwa ndio wazungumzaji wazuri wa Kiswahili.

Comments

Popular posts from this blog

Mambo Makuu Manne ya Kuzingatia ili Kufanya Upimaji Endelevu Wenye Tija

Mambo Muhimu ya Kuzingatia Katika Kuboresha na Kuongeza Ufanisi wa Shule.

Mambo Makuu Manne ya Kuzingatia ili Kufanya Upimaji Endelevu Wenye Tija-Sehemu ya Pili