Moja ya Matatizo Yanayoikumba Sekta ya Elimu ni Kukosekana kwa Uwajibikaji.


       Vyoo vya kutegemewa katika moja ya shule za sekondari hapa Tanzania
Madhara ya kukosekana kwa uwajibikaji

Uwajibikaji ni moja ya dalili kuu ya Uzalendo. Mtu aliye na sifa ya uzalendo, lazima awe muwajibikaji. Sekta nyingi hapa Tanzania zinashindwa kupiga maendeleo yenye tija kwa sababu mbalimbali, mojawapo na iliyo kuu ni kukosekana kwa uwajibikaji. Lengo la makala hii, ni kujadili viashiria kadhaa vya kukosekana kwa uwajibikaji na uwajibishwaji katika sekta ya elimu nchini Tanzania.
Wadau wote wa elimu kuanzia serikali na mamlaka zake husika, wakuu wa shule, walimu, wazazi/walezi, jamii na wanafunzi wenyewe wnahusika katika suala la uwajibikaji. Kila kundi lina nafasi yake na wajibu wake katika kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Muhusika wa kwanza anayepaswa kuwajibika ni mwanafunzi mwenyewe. Kuna ule msemo usemao, “unaweza kumlazimisha punda kwenda mtoni, lakini siyo kunywa maji”. Shule inaweza kuwa na mazingira rafiki ya kusomea, walimu wa kutosha na walio na vigezo, wawajibikaji na uongozi bora, na uwepo wa nyenzo muhimu za kusomea na kujifunzia,  lakini kama mwanafunzi hayupo tayari, ni bure kabisa. Mwanafunzi anapaswa kujitambua, kujua anahitaji nini na kwa namna gani atapata kile anachokihitaji.  Katika utafiti wake uliolenga kuangalia uhusiano uliopo kati ya kujitambua kwa mwanafunzi  na mchango wa wazazi unavyoweza kuathiri ufaulu wake, Bhat (2013) amegundua kuwa, mwanafunzi anapojitambua/ jielewa humpelekea kuwa na matokeo mazuri darasani.
Mtafiti huyu anatukumbusha kuwa, kuwasaidia wanafunzi kujitambua ni jukumu nyeti sana la serikali, wakuu wa shule, walimu, wazazi/walezi,  na jamii kwa ujumla. Uwekezaji wa kina wa kuhakikisha wanafunzi wanajitambua mapema kunaweza kuwa ni moja ya muarobaini wa kuondoa tatizo la matokeo mabaya ya mitihani mashuleni.
Bila kuwa na uwezo wa kujitambua, ni vigumu kupata wanafunzi watakaoweza kuelewa kuwa kuna upungufu wa vitabu katika shule yao, na hivyo kulazimika kutumia nguvu ya ziada, ikiwemo ya kuwa na moyo wa kusafiri umbali mrefu hadi shule nyingine ili kupata vitabu alivyovihitaji, au kufanya majaribio kadhaa ya maabara yaliyoshindikana shuleni kwake. Tatizo haliishii tu kwenye upungufu wa maabara au kukosekana kwa maktaba iliyojitosheleza (ni wanafunzi wangapi wanatumia maktaba za mikoa?), kwani hata masomo yasiyohitaji maabara, matokeo si ya kuridhisha. Mwanafunzi mwenyewe ni moja ya tatizo.
Wanafunzi wengi wa shule za msingi na sekondari wanahitaji mwongozo katika kujitambua. Kwa bahati mbaya sana, katika shule zetu, hakuna watu na ofisi maalum za ushauri nasaha. Mara nyingi, kitengo hiki muhumu hupewa mwalimu aonekanaye ana nidhamu nzuri ya kazi na busara. Hili ni tatizo kubwa, kitengo hiki kina watu mahususi ambao kwao ni kazi yao na wamebobea. Serikali haina budi kuwekeza katika hili. Hili likiwezekana, utakuwa ni mwanzo wa kupata jamii ya watu wanaojitambua, wawajibikaji (wanaokubali kuwajibishwa) na wazalendo.
Wazazi nao wana wajibu mkubwa sana katika kuhakikisha watoto wao wanafanikiwa katika masomo yao. Zipo namna nyingi ambazo mzazi anapaswa kuwajibika. Baadhi nimeshazigusia katika makala hii hapa. Hapa nitagusia wajibu uliopo kati ya mzazi na shule asomayo mwanae. Wazazi wanaonesha kutotimiza wajibu wao kwa kushindwa kuhoji shule husika kulikoni matokeo ya wanafunzi wao kuwa mabaya tofauti na matarajio yao. Kukosekana kwa uwajibikaji huu sio tu kwa wazazi lakini pia hata kwa mamlaka husika zinazosimamia elimu, wakuu wa shule na walimu husika wa masomo.
Kunapokuwa na matokeo mabovu, kila mmoja humtupia lawama aliye juu yake. Siyo mwalimu wa somo, siyo mzazi, siyo serikali, kila mmoja ananawa mikono. Hakuna anayetaka kujitazama wala kujiwajibisha, na hakuna wa kumuwajibisha mwingine. Siku za hivi karibuni, shule za serikali zimekuwa na matokeo mabaya. Wanafunzi wanamaliza elimu ya msingi bila kujua kusoma wala kuandika. Wazazi wanalipokea jambo hili bila kuhoji. Hawatimizi wajibu wao wa msingi. Walimu nao wanaona ni kawaida, mzazi aliyezaa atajua mwenyewe, nani kamwambia azae mtoto asiyeelewa.  Hafikiri kuwa anaweza kuwa sehemu ya tatizo.
Katika hali ya kushangaza, pamoja na ongezeko la shule nyingi za watu binafsi, ambazo zlilitegemewa kutoa huduma nzuri, baadhi ya shule hizi zimekuwa na matokeo mabovu.  Utozaji wa ada kubwa ni moja ya utambulisho wa shule hizi. Si wazazi, wala serikali inayoziwajibisha baadhi ya shule hizi zilizo na matokeo mabovu na miundo mbinu isiyofanana na matarajio ya wengi. Zipo shule binafsi zisizo na uongozi makini, walimu wenye vigezo, zisizo na maabara nzuri, maktaba na zisizowajali wafanyakazi wake lakini hakuna anayeziwajibisha wala yeyote kuwajibika.
Bila shaka wazazi huwapeleka watoto wao kwenye shule hizi bila kuzifahamu vyema huku wakiaminia uwezo wa vijana wao bila kujua kuwa, mazingira yanaweza kuathiri masomo yao. Kwa kutokujali, wazazi hupokea matokeo mabovu ya watoto wao na kutafuta namna nyingine ya kuwaendeleza, ikiwa ni pamoja na kumuwajibisha mototo. Mzazi anashindwa kufahamu pia, anapaswa kuihoji shule kufuatia matokeo mabovu ya mototo. Hii huweza kumsaidia mzazi kuchukua hatua sahihi dhidi ya mtoto wake.
Katika mtandao mmoja wa kijamii, nimekutana na madai ya walimu wanaodai kunyanyaswa na mwajiri wao kwa mkataba wao kuvunjwa bila kufuata taratibu. Mwajiri amekosa kuwajibika, nani amwajibishe? Wahusika wa kumuwajibisha wanalifahamu hili (kupitia mtandao wa kijamii?) kama kweli lipo?. Walimu nao wanawajibika lakini kwa njia ambayo siyo ya moja kwa moja. Kwa nini wasiende kwenye mamlaka husika? Pengine wameshaenda au wanajua namna wasivyo wawajibikaji, na hivyo wamehitaji nguvu ya wananchi na mwingine yeyote anayehusika ama kuguswa!
Moja ya idara muhimu za kujua mustakabali wa walimu na mazingira wanayofanyia kazi ni idara ya Ukaguzi wa shule. Wakaguzi wa shule ni kiungo muhimu kati ya shule, walimu na serikali. Idara ya ukaguzi ni moja ya idara muhimu sana katika kuhakikisha elimu bora inatolewa mashuleni, ikiwa ni pamoja na kulinda maslahi ya walimu. Shule binafsi zinapaswa kufikiwa na wakaguzi na wafanye kazi yao kizalendo. Watoe taarifa sahihi kwa kuzingatia uhalisia wa shule.  Serikali itemize wajibu wake wa kuziwajibisha shule za binafsi zinazowatoza wazazi ada kubwa bila kujali ubora wa elimu wanayotoa.
Mazingira ya kutokuwajibika ni mengi, kama haya ya shule ya Marasibora ya ukosefu wa vyoo, madawati na nyumba za walimu, yaliyoripotiwa na gazeti la Tanzania daima mapema mwaka huu mwezi wa nne. Inaonekana hakuna anayetaka kukubali kuwa hakuwajibika na hakuna akubaliye kuwajibishwa. 
Wakati mwingine, watumishi hupata kiburi cha kutowajibika kwa kuwa, mamlaka ya juu haijawajibika, yaani wanakomoa. Imefikia mahali sasa ule msemo wa “usiulize nchi yako itakufanyia nini, bali ujiulize wewe utaifanyia nini nchi yako”, umegeuzwa na kuwa, “wakati ninafikiri niifanyie nini nchi yangu, nayo nchi yangu haina budi kufikiri kama inanijengea mazingira sahihi ya kufikiri nitaifanyia nini”. Yawezekana msemo huu una mantiki. Akuandaliaye shibe usimkombee mboga. Hata mzazi, shibe ya njaa yake ni kuona kuwa watoto wake wameshiba. Tuwajibike, tukubali kuwajibishwa tunaposhindwa kujiwajibisha.

Comments

Yaani hata wangekosa darasa na kupata choo inasikitisha sana kwa kweli..
Albert Kissima said…
ndio Tanzania yetu hii Dada Yasinta. Bado tuna safari ndefu sana ya kuyapata maisha bora yanayoendana na hazina ya rasilimali tulizo nazo
Anonymous said…
educ is not a right to tanzanian as it is not stated in constitution rather its like a privilage that one can strive to get edu...under article (ii) in constituton lets fight for new constitution with the right to education to every citizen.

Popular posts from this blog

Mambo Makuu Manne ya Kuzingatia ili Kufanya Upimaji Endelevu Wenye Tija

Mambo Muhimu ya Kuzingatia Katika Kuboresha na Kuongeza Ufanisi wa Shule.

Mambo Makuu Manne ya Kuzingatia ili Kufanya Upimaji Endelevu Wenye Tija-Sehemu ya Pili