Mambo Muhimu ya Kuzingatia Katika Kuboresha na Kuongeza Ufanisi wa Shule.


Umbali kati ya shule na waishipo wanafunzi, hususani kwa shule za kutwa, umebainishwa na watafiti wa elimu kuwa unaathiri masomo ya mwanafunzi. Picha kutoka Fullshangwe Blog. Imetumiwa bila ruhusa.


Kama nilivyodokeza katika makala iliyotangulia, makala hii inajadili mambo kadhaa ya msingi ya kuzingatia ili kuboresha na kuongeza ufanisi wa shule, hususani za msingi na sekondari. Mambo haya ni matokeo ya tafiti mbalimbali za masuala ya uboreshaji na ufanisi wa shule. Ubora wa elimu Tanzania umeendelea kushuka siku hadi siku, na mikakati kadhaa ikiwamo ya matokeo makubwa sasa imeanzishwa katika kukabiliana na changamoto hii.. Harakati yoyote ya kuboresha ufanisi na ubora wa shule hauna budi kuzingatia mambo kadhaa yakiwemo haya takayoyajadili hivi punde kwa mujibu wa tafiti mbalimbali za kielimu.

Uongozi bora
Tafiti za masuala ya ufanisi wa shule zinaonesha kuwa, wakuu wa shule wamekuwa kiini cha mafanikio ya shule.  Tafiti hizi zinaonesha kuwa, ubora wao hufikiwa pale wanapotimiza majukumu yao ya kuhakikisha vifaa vya kufundishia na kujifunzia vinapatikana kwa wakati na vya kutosha, kueleza kwa uwazi dira na mikakati ya shule, kuelezea kwa uwazi na usahihi kile wanafunzi wanachotegemea kukipata wakati wa mafunzo yao, kuwa na mawasiliano rafiki,  ya mara kwa mara kati yake na walimu, wanafunzi, wafanyakazi wasio walimu, wazazi na jamii inayoizunguka shule. Pia, mkuu wa shule hana budi kutengeneza mazingira rafiki ya kufikiwa kwa urahisi na bila ya vikwanzo pale, mwalimu, mwanafunzi, mzazi au mwanajamii anapolazimika kuwasiliana naye ana kwa ana.
Mchango wa Wazazi na Jamii
Ogula na Asia(2013) katika kuchambua tafiti mbalimbali za masuala ya ufanisi wa shule, wamebaini kuwa, wazazi na jamii inayozunguka shule husika wana mchango mkubwa katika kuipatia shule mafanikio. 
Katika uchambuzi wao, wameonesha kuwa wajibu wa wazazi na jamii ni kuisaidia shule kifedha na kwa vifaa katika kuhakikisha shule inatimiza majuku yake ipasavyo, kushiriki kikamilifu kwenye safu za uongozi wa shule, kuwa na mawasiliano ya mara kwa mara kati ya uongozi na wafanyakazi wengine wa shule, kushiriki katika ufundishaji wa wanafunzi na shughuli nyingine za shule. Ikumbukwe kuwa, wazazi na wanajamii wanaweza kushiriki katika ufundishaji pale wanapokuwa likizo au baada ya kustaafu. Hili linawezekana, siyo tu kwa walimu, bali hata kwa kada nyingine kama vile madaktari wanaoweza kufundisha masuala mbalimbali ya afya ikiwemo na masomo ya sayansi kama vile bayolojia, kemia na fizikia.
Mbali na mambo hayo, jamii pia ina wajibu wa kuhakikisha inawaandaa vyema watoto wao ili waweze kupokea vyema yale wanayofundishwa shuleni. Katika kufaninikisha hili, wazazi, walezi na jamii hawanabudi kuhakikisha watoto wanapatiwa lishe ya kutosha, malazi bora, mavazi bora zikiwamo sare za shule, vifaa muhimu vya kujifunzia na kuhakikisha wanafunzi wanakuwa na afya njema wakati wote.
Uwezo wa Mwanafunzi wa Kujifunza.
Kama nilivyotanguliakusema katika  makala iliyopita, mwanafunzi mwenyewe ni sehemu muhimu ya kboresha au kushusha ufanisi wa shule. Tafiti za uboreshaji na ufanisi wa shule zimeweka bayana mambo kadhaa yamhusuyo mototo ambayo huweza kuathiri ufanisi wa shule husika. Mambo hayo ni pamoja na utayari wa mwanafunzi mwenyewe katika kujifunza maarifa na stadi mpya. Uongozi wa shule, walimu, wazazi na jamii hawana budi kujua namna bora za kuwaandaa watoto wao kisaikolojia ili wawe tayari kujifunza maarifa na stadi mpya, shuleni na majumbani.
Mambo mengine yanayomhusu mwnafunzi ni pamoja na mtazamo wake kuhusu shule, walimu na uongozi, hali ya uchumi wa nyumbani, maudhurio ya mwanafunzi shuleni na darasani, kiwango cha matarajio ya mwanafunzi kuhusiana na mustakabali wa elimu yake, umbali uliopo kati ya shule na aishipo mwnafunzi(husuani kwa shule za kutwa), nidhamu ya mwanafunzi husika ikiwa ni pamoja na historia yake ya matukio ya kinidhamu, shuleni na nyumbani.
Nidhamu kwa mwanafunzi ni moja ya nyenzo za muhimu sana katika kuhakikisha mwanafunzi husika na shule husika inafikia ,alengo yaliyokusudiwa. Kuna baadhi ya shule binafsi zimekuwa zikidahili wanafunzi walioshindikana kimaadili katika shule nyingine.  Bahati mbaya sana kama uongozi wa shule na walimu hawatakuwa na historia sahihi ya wanafunzi hawa, wanaweza kupoteza muda mwingi kukabiliana na matatizo ya kinidhamu. Upotezaji wa vipindi kwa ajili ya kukaa vikao vya nidhamu unaweza kuathiri ufanisi wa shule kwa kiasi kikubwa, na hivyo kuzuia kufikiwa kwa malengo ya shule.
Sio lengo langu kusema kuwa wanafunzi wenye historia mbaya ya nidhamu wasipokelewe mashuleni, la hasha. Lengo hapa ni kuukumbusha uongozi pamoja na walimu kufuatilia vyema historia za wanafunzi, hususani kwa shule zenye mazoea ya kuchukua wanafunzi wanaoendelea na masomo kutoka katika shule nyingine. Utaratibu huu utawawezesha walimu na uongozi kutumia mbinu sahihi katika kuwakuza vijana hawa kimasomo, kimaadili na kijamii.
Kufuatilia uwezo wa mwanafunzi mmoja mmoja husaidia pia kufahamu wanafunzi wanaohitaji uangalizi maalum. Kwa mfano, wapo watoto wanaohitaji matunzo maalum kama vile wenye usikivu hafifu, wasioongea n.k. Pia, kufahamu historia ya maisha ya mwanfaunzi akiwa nyumbani na utamaduni wake huweza kusaidia katika kuelewa namna bora ya kumkuza kitaaluma na kijamii.
Muda ambao Mwanafunzi anaoutumia Kujifunza awapo shuleni na Nyumbani.
Kwa mujibu wa tafiti zilizofanyika za ufanisi na ubora wa shule katika nchi za ulimwengu wa tatu na zinazondelea, imeonekana kuwa, ,kuna uhusiano mkubwa kati ya mafanikio ya mwanafunzi kielimu pamoja na muda anaoutumia katika kujifunza. Tafiti nyingi zinaonesha kuwa, wanafunzi wanapotumia siku nyingi za mwaka  wakiwa shuleni na wakijibidisha na kazi zilizoandaliwa na kuratibiwa vizuri na walimu hao, hufanya vizuri zaidi katika masomo yao. Imefahamika pia kuwa, utoaji wa kazi nyingi za nyumbani kunakomfanya mwanafunzi awapo nyumabani atumie muda wake vizuri katika masomo, kuwemekuwa na matokeo chanya katika ufaulu wa wanafunzi. Pia, muda mwingi wa ufundishaji madarasani umeonekana kuongeza kiwango cha ufaulu wa wanafunzi.
Kwa bahati mbaya, katika shule zetu za msingi na sekondari, kumekuwa na uvunjwaji wa vipindi mara kwa mara na hivyo kumega siku nyingi ambazo mwanafunzi alipaswa kujifunza. Baadhi ya mambo ambayo yamekuwa yakimega muda wa wanafunzi wa kujifunza darasani na walimu kufundisha ni vikao visivyokuwa na muda maalum na vinavyofanyika wakati wa masomo, shughuli zisizokuwa na ulazima kwa wanafunzi kama vile kufanya kazi kwa  walimu n.k
Mambo mengine ya kuzingatia katika kuleta ufanisi wa shule ni pamoja na kuangalia uwezo wa walimu. Uwezo wa mwalimu hujumuisha mambo kadhaa kama vile uzoefu wake, kiwango cha elimu, kuangalia kama mwalimu ametimiza matakwa ya kuwa katika taaluma yake, utayari wa mwalimu katika kufundisha, ujuzi wa kutahini na kutathmini wanafunzi, tabia ya uhamaji wa mwalimu kutoka shule moja hadi nyingine,  uwiano wa mwalimu na wanafunzi katika darasa n.k
Pia, tafiti hizi zinaonesha kuwa ubora wa ufundishaji unachangia kupata matokeo chanya ya wanafunzi na hivyo kuboresha ufanisi wa shule. Ubora wa ufundishaji katika tafiti za kielimu zilizokwisha fanyika zimezingatia mambo kama vile ubora wa mbinu na njia za ufundishaji, uwezo wa mwalimu katika somo analofundisha, mtazamo wa mwalimu kuhusu wanafunzi na shule, ikiwa ni pamoja na kuwa na utayari wa kufanya kazi kwa moyo na kuitumikia shule kwa kuzingatia mikakati na dira ya shule, utoaji wa mazoezi na kazi za nyumbani mara kwa mara na urudishaji wa haraka wa matokeo.
Uungwaji Mkono Kutoka  Mamlaka za Elimu
Tafiti nyingi za kielimu zinaonesha kuwa, mamlaka za elimu zina mchango mkubwa katika kuhakikisha  ubora na ufanisi wa shule unafikiwa. Mamlaka hizi ndizo zinazopaswa kuhakikisha walimu wanapata maslahi yao ya kutosha na  kwa wakati, wanapata mazingira rafiki ya kufundishia na wanafunzi wanapata mazingira rafiki ya kujifunzia na kuhakikisha kuna zana bora na za kutosha za kufundishia na kujifunzia.
 Kwa kawaida wakaguzi wa shule wamekuwa ndio kiungo kikuu kati ya shule na mamlaka za juu za elimu. Wakaguzi wa shule wana majukumu ya kufuatilia mchakato wa ufundishaji na ufundishaji mashuleni na kuwashauri walimu na wakuu wa shule katika mambo kadhaa yanayolenga kuongeza ufanisi na ubora wa shule. wanajukumu pia la kuleta mrejesho wa changamoto wanazoziwasilisha katika mamlaka za juu za elimu. Kwa Tanzania, wakaguzi wa shule hawajapewa msisitizo wa kutosha.  Upitiaji wa shule umekuwa wa mara chache sana. Pia, mrejesho wa mambo kadha wa kadha umekuwa haufanyiki na hivyo, kitengo hiki muhimu kuonekana kutotimiza wajibu wake ipasavyo.
Kwa upande mwingine, walimu wengi wamekuwa wakiwaogopa wakaguzi wa shule kutokana na sababu kadhaa ikiwemo ya kujengeka kwa dhana miongoni mwa walimu wengi kuwa, wakaguzi huja kuhukumu badala ya kushauri na kuelekeza yapi yafanyike. Bila shaka, kukosekana pia kw maadili ya kazi miongoni mwa walimu mara kw mara, kunaweza kuchangia wakaguzi hawa, pindi wafikapo mashuleni kuchukua hatua kali zaidi kutokana na ukiukwaji wa taratibu za kazini kujirudia siku hadi siku.
Mambo haya niliyoyajadili ni ya muhimu kuzingatiwa katika kuhakikisha ubora na ufanisi unaotakiwa katika shule yetu yanafikiwa. Ikumbukwe pia kuwa, haya ni baadhi, yapo mengi kwa kuzingatia pia kuwa, tafiti za kielimu zinaendelea kufanyika na mambo mengine mengi yanaweza kuibuliwa mbali na hay machache niliyoyajadili. Kama nilivyotangulia kusema, mambo haya yataweza kuleta ufanisi mkubwa kama tu kila mmoja atawajibika kwa nafasi yake. Hivyo basi, makala inayofuata, itaangalia kwa ufupi, suala hili la uwajibikaji katika kuhakikisha ubora na ufanisi unaotakiwa wa shule unafikiwa.

Shukrani kwa Ogula na Rubeba (2013) walioandaa makala ya Mapitio ya Tafiti za Kielimu za Uboreshaji na Ubora wa Shule iliyochapishwa katika Jarida la Tafiti za Kielimu, toleo la kwanza, la Chuo Kikuu cha Kikatoliki Cha Mwenge.Comments

Christian Bwaya said…
Kisima, huu ni mfano bora kabisa wa matumizi sahihi ya elimu katika kuyachambua matatizo yanayotukabili na kuleta mapendekezo sahihi na sio kuishia kulalamika. Hongera sana kaka.
Albert Kissima said…
Shukrani saaaana kaka. Ninafurahi sana kutambua kuwa unafuatilia hiki nikiandikacho, ninapata faraja na hamasa ya kipekee kabisa ya kuendelea kuwashirikisha kile niaminicho kitawafaa watanzania na Dunia kwa ujumla. Karibu sana kaka.
Unknown said…
Maoni na mtazamo wako katika kuboresha kiwango cha ufaulu katika elimu nchini ni mzuri na uliotazama umuhimu wa kila mdau katika kuufikia ufanisi. hongera sana
Unknown said…
Safi sana umefafanua vizuri hakika utaisadia jamii pamoja na walimu.

Popular posts from this blog

Mambo Makuu Manne ya Kuzingatia ili Kufanya Upimaji Endelevu Wenye Tija

Mambo Makuu Manne ya Kuzingatia ili Kufanya Upimaji Endelevu Wenye Tija-Sehemu ya Pili