Tunazingatia matumizi ya Lazima na Hiari kwa pato letu?

Ni mda mrefu ulipita sikuonekana katika ulimwengu huu wa ku-blogu. Nilibanwa na baadhi ya majukumu, na sasa nimerudi tena na tupo pamoja. Niombe radhi kwa kutokuweka wazi juu ya adimiko langu.Naam, wakati wa adimiko, nilipata kujifunza mengi, na leo naona ni vema nigusie kidogo matumizi ya pato la mtanzania mmoja mmoja na mchango wake katika kuendeleza wimbi la umasikini au kuweza kujikwamua na umasikini.Popote pale Tanzania, mjini na vijijini, asilimia kubwa ya watanzania wenye uwezo wa kufanya kazi huonekana katika pilikapilika za hapa na pale. Wapo wafanyao kazi halali na wale wasiofanya kazi halali, lakini mwisho wa siku kila mmoja anapata ujira wake.Wapo waliojiajiri na pia walioajiriwa. Waliojiajiri, mwisho wa siku huweka chao kibindoni na wale walioajiriwa husubiri mwisho wa mwezi ndipo waweke chao kibindoni. Maisha haya humgusa yeyote yule ambaye si tegemezi katika familia au sehemu aishiyo.Huko mijini, watu huonekana kila mmoja na pilika yake ilimradi mkono uingie kinywani. Kila aina ya kiwezekanacho kufanyika hufanyika. Wapo wafanyabiashara wakubwa, wafanya biashara ndogondogo kama wamachinga, wang'arisha viatu, wauza karanga, wauza maji n.k na wale wa maofisini. Vijijini nako hali kadhalika, watu na pilika zao. Kote huku, ni imani yangu kuwa kila mmoja anapata ujira wake, mdogo, usioridhisha na pia wapo wanaopata pato kubwa na la kuridhisha.


Ninachojiuliza hapa ni kuwa; pato la kila mmoja hulitumia ipasavyo? Watu huwa na malengo sahihi ya pato lao?Matumizi yetu yanalenga mambo ya lazima na kuacha kupoteza pato letu kwa mambo ya hiari (yasiyo ya lazima)?.Wapo watu wahangaikao mchana kutwa kutafuta pesa na usiku huzitumia kujiburudisha kwa kunywa pombe, kuhongea wanawake/wanaume, uvutaji bangi, n.k na asubuhi huamka bila hata shilingi moja na huanza kutafuta tena, na utaratibu unakuwa ndio huo huo miaka na miaka. Hata wale wasubiriao mshahara mwisho wa mwezi, hulimbikiza madeni kwa mtumizi yasiyo ya lazima na mwisho wa mwezi hujikuta wanamalizia mshahara wao kwa kulipa madeni ya mtumizi ambayo hayakuwa na ulazima.Kwa mwenendo huu, ni dhahiri maendeleo hayatapatika na kama yatakuja, basi ni kwa pole pole sana.Wapo wengi waishio maisha haya, na hali hii imechangia sana watu kuishi katika hali duni ya kimasikini.Wapo wazingatiao matumizi sahihi ya kipato chao kwa kutoa kipau mbele kwa mambo ya lazima na kutotoa nafasi kwa mambo ya hiari,yale yasiyo ya lazima. Kwa kiasi kikubwa, watu husonga mbele kimaendeleo, kwani kila kukicha hupiga hatua kadhaa za kimaendeleo kwa kutimiza kwanza mambo yao ya lazima, yaani yale yenye umuhimu stahiki yakilinganishwa na mengine.Matumizi ya lazima na hiari kwa kipato chetu, binafsi nadhani ni miongoni mwa nyenzo muhimu sana zitakazo tusaidia kupigana na adui umasikini. Wengi tuna utajiri wa kujituma lakini wengi wetu tuna umasikini wa namna sahihi ya kutumia kipato chetu kidogo ama kikubwa.Hakuna haja ya kuanza kununua soksi wakati hatuna kiatu, vilevile, haitakuwa busara kuanza kununua nguo ya ndani wakati hatuna suruali,itakuwa haina maana.
Tuyape kipau mbele mambo ya "lazima" na tuwe makini na utumiaji wa pato letu kwa mambo ambayo ni ya "hiari" ambayo kutoyatimiza hakutapelekea mabadiliko yoyote chanya katika maisha yetu, bali yatazidi kutudidimiza kwenye dimbwi la umasikini.

Comments

Ambaye hataweza kusoma TOLEO ZIMA, basi angalau achukue AYA hii
"Hakuna haja ya kuanza kununua soksi wakati hatuna kiatu, vilevile, haitakuwa busara kuanza kununua nguo ya ndani wakati hatuna suruali,itakuwa haina maana.
Tuyape kipau mbele mambo ya "lazima" na tuwe makini na utumiaji wa pato letu kwa mambo ambayo ni ya "hiari" ambayo kutoyatimiza hakutapelekea mabadiliko yoyote chanya katika maisha yetu, bali yatazidi kutudidimiza kwenye dimbwi la umasikini."

KARIBU TENA KAKA
Kwa hakika tulikosa busara zako
Albert Kissima said…
Nashukuru sana kaka Mubelwa.
Gabriel paul said…
Huu ni ukweli ulio wazi.nahisi kila anayesoma hapa anaona tayari alishawahi kukosea.uzuri kujirekebisha inawezekana.natamani basi hata serikali yetu ingeweza kutumia busara hizi katika utendaji.mengi serikali ilikosea kwa kushindwa kujua nini ni muhimu na matokeo yake tumeangukia kwenye maisha yaliyo na mfumuko wa bei kila siku wakati mishahara haiongezeki matokeo yake wananufaika wachache na wengi wanaishia kwenye umaskini wa kutupwa.NASHUKURU SANA KWA CHANGAMOTO ULIYOITOA.NAFIKIRI KWA WENGI HAPO ITAKUKUWA NDIO PAKUANZISHA MWENDO TENA KASI WA KIMAENDELEO.
Albert Kissima said…
Kaka Gabriel, umesema vyema, serikali nayo haina budi kufuata kanuni hii ya mambo ya lazima na hiari ili iepukane na upotezaji wa fedha nyingi kwa mambo yasiyo na tija kwa taifa na kwa wananchi.

Popular posts from this blog

Mambo Makuu Manne ya Kuzingatia ili Kufanya Upimaji Endelevu Wenye Tija

Mambo Muhimu ya Kuzingatia Katika Kuboresha na Kuongeza Ufanisi wa Shule.

Mambo Makuu Manne ya Kuzingatia ili Kufanya Upimaji Endelevu Wenye Tija-Sehemu ya Pili